Mgombea urais wa CCM, Dkt John Magufuli ameligeukia jiji la Dar es Salaam ambalo ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa lengo la kusaka kura za ushindi.

Dkt. Magufuli anaanza leo kampeni zake katika majimbo ya Dar es Salaam ambapo atafanya mikutano katika maeneo ambayo aliyaacha pale aliozulu jiji hilo hivi karibuni na kufanya mikutano kadhaa ya kampeni.

Kwa mujibu wa ratiba ya NEC, Dkt. Magufuli atatumia siku tatu kufanya kampeni katika maeneo ya Kigamboni, Temeke, Mbagala, Ilala, Segerea, Kibamba, Kawe na Kinondoni ambapo atatumia nafasi hiyo pia kuwanadi wagombea ubunge na udiwani wa maeneo husika.

Baada ya kukamilisha kampeni zake jijini Dar es Salaam Oktoba 23, Dkt. Magufuli na viongozi wa CCM wanatarajiwa kufunga kampeni zao Oktoba 24 katika jiji la Mwanza, tukio linalotarajiwa kuvunja rekodi na kuacha historia kubwa kwani ni siku watakayokuwa wakirusha karata yao ya mwisho katika kuwashawishi watanzania kumchagua Dkt. Magufuli na wagombea wa CCM.

Akiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa alipokamilisha ziara yake jana, Dkt. Magufuli alisema kuwa watanzania wakimchagua ataleta mabadiliko ya kweli kwa kuongeza ajira na kufanya mapinduzi ya kiuchumi kupitia viwanda.

Aliahidi kuwa serikali yake itaboresha maslahi ya wafanyakazi wa serikali pamoja kuboresha mfumo wa utendaji katika serikali kwa maslahi ya Umma, huku akipambana na ufisadi na wizi wa fedha za umma.

 

Rais Wa Syria Afanya Ziara Ya Ghafla Urusi Huku Ndege Za Marekani Zikielekea Kwake
Mourinho Ajiweka Kikaangoni UEFA