Rais John Magufuli leo aliungana na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuzindua ujenzi wa barabara ya kilometa 234.3 kutoka Arusha (Tanzania) hadi Hilolo (Kenya) huku akieleza kuwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawahitaji vyama vya siasa bali maendeleo.

Rais Magufuli alieleza kuwa ujenzi huo wa barabara ni hatua muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Jumuiya hiyo ambao shida yao sio vyama vya siasa bali ni kuona uchumi wao unakua na hali ya maisha inazidi kuboreka.

“Watanzania wa Arusha na Wanzania wa Tanzania yote na watu wote tulio ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunachokihitaji sio mavyama vyama. Watu wanahitaji maendeleo. Watu wanahitaji wale vizuri, wapate ajira, wawe na maisha mazuri. Mambo ya kuombaomba yaishe… na mambo ya kuwafanya wachache wanakuwa na mali sana halafu wengi wanabaki masikini nayo yaishe,” alisema Rais Magufuli.

Alieleza kuwa lengo lake na viongozi wenzake wa Afrika Mashariki ni kuhakikisha kuwa maisha ya wananchi wa Jumuiya hiyo yanazidi kuboreka.

Naye Rais wa Kenyatta alieleza kuwa mipaka ya nchi ni suala linaloangaliwa zaidi na viongozi wa kisiasa lakini wananchi hawahitaji mipaka hiyo kwani hupenda kuvuka na kufanya biashara kati ya nchi hizo bila kujali mipaka hiyo.

Alisema kuwa miundombinu inayounganisha nchi hizo ni suala muhimu litakaloziunganisha nchi hizo bila kujali mipaka yake ili kuwawezesha wananchi kukuza uchumi kwa kutumia fursa zilizopo.

“Sisi kama serikali ndio tumefanya kazi ya kulala wakati kumekucha. Tumelala kwa sababu, wananchi wako mbele yetu… wananchi hufanya kazi pamoja, hufanya biashara pamoja, huvuka mipaka kwenda huku na kurudi,” alisema Rais Kenyatta.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisisitiza kuwa Afrika Mashariki sio masikini kama inavyoelezwa kwani kuna rasilimali nyingi na utajiri mkubwa hivyo kwa kutumia fursa zilizopo na kuunganisha miundombinu, hali ya maisha itaboreka.

Barabara hiyo inayotoka Arusha kwenda Holili nchini Kenya, inagharimu zaidi ya shilingi bilioni 200.

Korea Kaskazini kufanya shambulizi la bomu la Nuclear
Wauguzi 'wanusa moto' baada ya mzazi kujifungulia kwenye beseni akiwa hospitalini