Mgogoro wa uchaguzi wa marudio wa Zanzibar umekosa kimbilio la kupata maridhiano baada ya Rais John Magufuli aliyekuwa akitajwa mara kadhaa kuwa ndiye angeweza kuumaliza, kutangaza rasmi kujiweka kando.

Akiongea jana na wazee wa Dar es Salaam, Rais Magufuli alieleza kuwa hana uwezo wa kuingilia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar kwakuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)  ni huru na haipaswi kuingiliwa kwa mujibu wa katiba.

Rais Magufuli alieleza kuwa wanaolalamikia tafsiri ya katiba na sheria kuhusu kufutwa kwa matokeo na kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio, waende kuomba tafsiri hizo mahakamani.

“Kuhusu Zanzibar, kama tume za uchaguzi nyingi duniani, haiwezi kuingiliwa na Rais yeyote ndiyo maana tume za uchaguzi huwa huru. Napenda kuheshimu sheria,” alisema Magufuli.

“Hiyo ZEC ina uhuru wa kuamua mambo yake lakini kama kuna tafsiri mbaya, waende mahakamani, mahakama ziko pale halafu unamwambia Magufuli ingilia,” aliongeza.

Alisema kuwa jukumu lake kama Amiri Jeshi Mkuu ni kuhakikisha kuwa  kuna amani na utulivu nchini huku akiwaonya wale wote wanaopanga kuvuruga amani visiwani humo.

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana akieleza kuwa uligubikwa na kasoro nyingi. Baadae alitangaza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika Machi 20 mwaka huu.

Mazungumzo ya kutafuta maridhiano kati ya wapinzani wakuu, Dk. Ali Mohammed (CCM) Shein na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) yalishindikana, huku Maalim Seif akimuomba Rais Magufuli kuingilia kati.

Awali, wagombea hao walikutana na Rais Magufuli kwa nyakati tofauti  Ikulu jijini Dar es Salaam kumuelezea kuhusu mazungumzo yanayoendelea kutafuta muafaka na Rais alieleza kuridhishwa na hatua waliyoifikia.

 

 

Kingunge avunja ahadi yake kuhusu Magufuli
Mwanamke aliyewanyang'anya majambazi Bunduki agomea zawadi ya pesa za Polisi