Zikiwa zimebaki siku 44 watanzania waamue nani apewe ridhaa ya kuwa rais wa Tanzania, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli ameendelea kuchanja mbuga huku akisisitiza kuwa atafuta posho na sherehe zisizokuwa na tija.

Jana, mgombea huyo alifanya mkutano mkubwa wa kampeni mjini Korogwe ambapo aliwataka wananchi wamchague kwa kuwa atahakikisha anaokoa fedha nyingi za umma zinazopotea kwa kufuta baadhi ya sherehe, posho na semina zinazotumia fedha nyingi huku miradi ya maendeleo ikikwama.

“Nashangaa kwenye jimbo hakuna maendeleo huku unasikia kuna wiki ya maji, sijui wiki ya mbuzi, wiki ya kunyonyesha… nitafuta,” alisema.

Katika hatua nyingine, Magufuli aliwataja sifa za mawaziri wa serikali atakayoiongoza endapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania.

Alisema mawaziri atakaowateua lazima wawe wachapakazi wenye lengo la kuwatumikia wananchi bila kujali muda wa kazi. Pia, alisema ili mtu awe waziri katika serikali yake ni lazima asiwe bingwa wa kutoa visingizio katika kuhalalisha ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi.

“Nitaweka aina ya mawaziri ambao wao ni kazi tu, wakipelekewa matatizo ya wananchi wanayatatua kw wakati na sitaki kusikia visingizio kama mchakato unaendelea wala nini,” alisema.

Dk. Magufuli aliendelea kuahidi kufufua viwanda vya ushirika kwa kuwa serikali yake itakuwa serikali ya viwanda itakayotoa ajira nyingi kwa watanzania.

Mgombea huyo ambaye anaongozwa na kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, anaendelea na kampeni zake huku mikutano yake ikishuhudiwa kuwa na umati mkubwa.

Petit: Mpaka Leo Ninajutia Kusajiliwa Na Chelsea
Prince Ali Atangaza Kurejea FIFA