Mgombea urais kupitia CCM, Dkt. John Magufuli jana alilitikisa jiji la Mwanza baada ya maelfu ya wakazi wa mkoa huo kufurika katika viwanja vya Furahisha kumsikiliza.

Dkt. Magufuli ambaye aliwasili katika uwanja wa ndege wa Mwanza majira ya mchana akitokea Dar es Salaam alilakiwa na umati mkubwa wa wananchi waliopanga foleni pembeni mwa barabara hadi katika uwanja wa Furahisha.

Mbwembwe zilitawala ambapo baadhi ya wanawake walitandika khanga chini ya barabara ili mgombea huyo apite. Vijana nao walionekana wakifagia na kudeki barabara huku wengine walilala katikati ya barabara na kusababisha kazi ya wana usalama kuwa ngumu zaidi.

Msafara wa Mgombea huyo ulichukua muda kufika katika viwanja hivyo kwa kulazimika kwenda kwa mwendo wa taratibu kutokana na idadi ya watu waliokuwa barabarani huku wengine wakitaka kumsalimia. Burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wakubwa wa muziki wa Bongo Flava kama Temba na Chege ilisindikiza tukio hilo na kuwapa burudani wahudhuriaji kabla ya kumsikiliza mgombea huyo.

M

Akizungumza na wananchi hao, Magufuli alieleza kufurahishwa na mapokezi hayo na kudai kuwa hayajawahi kutokea katika maeneo yote aliyopita katika kipindi hiki cha kampeni na kudai kuwa yamevunja rekodi ya Afrika.

“Kwa kweli wananchi wa Mwanza mmenishangaza kwa mapokezi haya makubwa. Ingawa kote nilikopita hali ni hivi hivi, lakini ninyi mmetia fora sio tu Tanzania na Afrika nzima hayajawahi kutokea,” alisema Dkt. Magufuli.

Mgombea huyo aliwaahidi wananchi wa mkoa huo kuwa hatawaangusha katika kipindi cha utawala wake endapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania huku akidai tayari ameshakuwa rais kwa kuwa watanzania wameshaamua kuwa wote watampigia kura.

Aliwaahidi wananchi wa mkoa huo kuwa atahakikisha anatekeleza ahadi aliyoitoa rais Jakaya Kikwete ya kununua meli mpya. Pia, aliahidi kujenga barabara za juu maarufu kama flyover pamoja na kufufua viwanda katika jiji hilo.

Alisema kuwa kwa kuwa serikali yake itakuwa ya viwanda, atahakikisha anafunga umeme wa KV 400 na kuunga na mkongo wa Taifa.

Msafara wa Magufuli

“Magufuli anakuja na mabadiliko ya kweli kupitia uchumi wa viwanda, na kutokana na hilo tutafunga umeme wa KV 400 ambazo tutaunganisha na gridi ya taifa,” alisema.

Alisema atabadili jiji la Mwanza kuwa Geneva ya Afrika kwa kuwa jiji hilo ni jiji la kiuchumi kutokana na jiografia ya jiji hilo kuwa karibu na nchi kadhaa za Afrika. Aliongeza kuwa atahakikisha anafanya mabadiliko makubwa katika jiji hilo kwa kuwa yeye ni mwenyeji na aliwahi kuishi hapo kwa kipindi kirefu hivyo analifahamu vizuri.

Aliwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza kumpigia kura za ndio bila kujali vyama vyao kwa kuwa atakuwa rais wa watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, dini au kabila.

“Mzee Mkapa aliniita askari namba moja wa mwamvuli, naye Rais Jakaya Kikwete akaniita tingatinga, sasa nichagueni nitinge hadi Ikulu,” alisema na kuongeza kuwa anao uzoefu mkubwa na haombi kazi ya urais kwa kufanya majaribio.

 

Magufuli Kuwezesha Tafiti Kuinua Uchumi
Kingunge Aeleza ‘Kosa Kubwa’ Linalofanywa Na CCM Kwenye Kampeni Mwaka Huu