Siku kadhaa baada mwandishi nguli, Jenerali Ulimwengu na askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kumkosoa Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete kwa kauli kali, Rais John Magufuli amejibu akimhakikisha amani mstaafu huyo.

Hivi karibuni, Jenerali Ulimwengu alisema kuwa Dk. Kikwete anatakiwa kushtakiwa kwa kupoteza mabilioni ya shilingi za umma kupitia mchakato wa katiba mpya ambayo haikukamilika. Naye Askofu Gwajima alidai mengi yaliyotumbuliwa na Rais Magufuli yanamhusu mstaafu huyo.

Akizungumza jana wakati akipokea ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rais Magufuli alimtaka Dk. Kikwete na marais wote wastaafu kutosikiliza ‘kelele’ na mambo aliyoyaita ya ‘ovyo-ovyo’ kwakuwa atawalinda.

“Mjue mimi mtoto wenu nipo. Watachonga lakini nataka kuwahakikishia kuwa mtaishi kwa amani. Mengini hata mkiyasikia, tupa pembeni kwa sababu mimi ni kiongozi wenu mwenye jukumu la kuliongoza Taifa hili nipo pamoja nanyi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuwa anashangaa wanaodai kuwa Dk. Kikwete anapaswa kushtakiwa wakati hata yeye alikuwa miongoni mwa walioshiriki katika hatua mojawapo ya mchakato wa kupata katiba hiyo lakini hawajasema ashtakiwe.

“Mbona mimi nilikuwamo lakini hawajasema nishtakiwe? Alihoji Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliahidi kuendelea na mchakato wa katiba mpya kuanzia pale ulipoishia kwani ilikuwa vigumu kuendelea wakati kulikuwa na jukumu zito la uchaguzi Mkuu. Hivyo, alisema kuwa Serikali itashirikiana na NEC kuhakikisha mchakato huo unakamilika na watanzania wanapata Katiba Mpya.

Arsene Wenger Amekubali Kushindwa
Uingereza Kuondoka EU?