Zikiwa zimebaki saa kadhaa Tanzania iamue nani atakayekuwa rais wa serikali ya awamu ya tano, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli amezikosoa vikali kauli za mshindani wake mkubwa, Edward Lowassa wa Chadema.

Akiongea katika moja ya kampeni zake jijini Dar es Salaam katika siku za lala salama, Mgombea huyo wa CCM alizikosoa bila kutaja jina, kauli ya kuhamisha fedha zilizotengwa kujenga bandari mpya ya Bagamoyo ili zikafufue kwanza bandari ya Tanga.

Dkt. Magufuli alisema kuwa kauli hizo ni za kujenga chuki kati ya wananchi wa Tanzania kupitia mgawanyo wa rasilimali walizonazo. Alisema kuwa kauli hizo hazifai na zinasikitisha kutolewa na watu wanaotaka madaraka makubwa nchini. aliwatahadharisha wananchi kutokubali kumuunga mkono kiongozi anayetoa kauli hizo.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa akiingia madarakani ataendeleza ujenzi wa bandari hiyo Bagamoyo, “haya sasa naingia mimi Magufuli sio mtu wa Bagamoyo, lakini nasema ntajenga bandari ya Bagamoyo.”

Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, akiwa jijini Tanga hivi karibuni, aliahidi kuwa ataangalia uwezekano wa kurudisha fedha zilizotengwa kujenga bandari ya Bagamoyo ili zifufue bandari ya Tanga.

“Tatizo kubwa la Tanga halina ajira, na hii inatokana na viwanda vyote vilivyokuwepo vimekufa vimefilisiwa. Bandari haina kazi, lakini hivi karibuni zimetolewa pesa nyingi sana kupelekwa bandari ya Bagamoyo. Mimi nasikitika, kwa maoni yangu, fedha hizo zingeletwa kufufua bandari ya Tanga. Kuna mamilioni ya pesa, yangeletwa, kila mtu wa Tanga angepata kazi, alisema Lowassa.

“Lakini zimepelekwa Bagamoyo, sijui kwa vigezo gani. Lakini serikali yangu itaangalia uwezekano wa kufuta huo mkataba hizo pesa zije hapa zifufue bandari kwanza,” aliongeza.

 

Van Gaal Akiri Kuzidiwa Na Mzigo Old Trafford
Ronaldo Aanza Kumgaragaza Messi Kabla Ya 2016