Wakati sakata la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kumtupia vilago Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe kwenye jengo lake jijini Dar es Salaam kwa madai ya kutolipa kodi ya pango ya shilingi bilioni 1 likiendelea, Rais John Magufuli amelitaka shirika hilo kutolegeza kamba.

NHC ilimfukuza Mbowe kwa kumtolea nje vifaa vyake kwenye jengo lililokuwa na biashara za club Bilicanas pamoja na ofisi za kampuni ya Free Media ambayo ni mchapashishaji wa gazeti la Tanzania Daima. Hata hivyo, Mbowe amekana kudaiwa ‘hata senti’ na shirika hilo na kuahidi kuliburuza mahakamani.

Akituhubia jana jijini Dar es Salaam baada ya kukagua ujenzi wa Jengo la hostel litakalobeba wanafunzi zaidi ya 3840 kwa pamoja katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Rais Magufuli alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo kuendelea kuwatupia nje vilago wadeni sugu kama alivyofanya kwa Mbowe, ingawa hakumtaja jina.

“Wapangaji wote wa Serikali, Wizara gani kule…ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni yao, wasipolipa endelea kuwatoa nje kama ulivyomtoa yule jamaa,” alisema Rais Magufuli.

Alilitaka shirika hilo kutomuonea haya mtu yoyote ambaye hajalipa kodi ya pango bila kujali wadhifa wake na itikikadi yake kisiasa.

“Endelea hivyo hivyo. Usiogope kumtoa nje mtu yoyote. Awe amepangishwa ni wa CCM, mtoe nje, awe ni wa Ukawa mtoe nje, awe Serikali mtoe nje, awe Waziri mtoe nje, awe mpangaji huyo ni Rais mtoe nje,” alisema.

Rais Magufuli alisema kuwa ili shirika liendelee, ni lazima lihakikishe kuwa linakusanya kodi ya pango kadri iwezekanavyo.

Majengo ya nyumba za Hostel hiyo ya Serilai kubwa zaidi chuoni hapo yanatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu.

Mtatiro aukataa uenyekiti wa CUF, Atangaza chama kujiunga na UKUTA
Apandishwa kizimbani kwa kumtishia Magufuli kwenye WhatsApp