Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais wa serikali ya awamu ya tano, atafuata nyayo za waliomtangulia ili aweze kuwatumikia wananchi vyema na kuleta maendeleo ya kweli.

Dk. Magufuli aliongea hayo jana wakati akifanya mikutano ya kampeni mjini Iringa, ambapo alieleza kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya wazee ambayo ataitumia vyema pale anapohitaji ushauri kwa maendeleo ya taifa.

“Natamka hapa, baba yangu alishafariki dunia, lakini najivunia sana mzee Mwinyi, Mkapa, Salim, Warioa na huyu mzee Malecela, hawa watakuwa kimbilio langu kama nitachaguliwa kuwa rais,” alisema Magufuli.

Katika hatua nyingine, Magufuli alisifia kazi iliyofanywa na rais Jakaya Kikwete na kueleza kuwa wanaobeza safari zake wanapaswa kupuuzwa kwa kuwa safari hizo zimeleta matunda kwa taifa. Alisema kutokana na safari za rais Kikwete za hivi karibuni, serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Milenia (MCC), limeipatia Tanzania shilingi bilioni 992.8 ili kusaidia sekta ya umeme nchini.

Mgombea huyo wa urais kupitia CCM, leo anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni mjini Dodoma ambayo ni moja kati ya ngome ya chama chake.

 

CCM Yamtimua Mwandishi Wa Mwananchi Kwenye Timu Ya Wana Habari, Kisa…
Pellegrini Angewashuhudia Man City Kideoni