Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameeleza sababu zilizopelekea kuzifutilia mbali shamrashamra za sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara mwaka jana na kuamuru iwe siku ya usafi.

Rais Magufuli alizifuta sherehe hizo mwaka jana na kuagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shamrashamra zitumike kutengeneza barabara ya Ali Hassan Mwinyi (Mwenge-Morocco) jijini Dar es Salaam.

Akihutubia jana katika shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 55 ya uhuru wa Tanzania bara zilizofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli ameeleza kuwa sababu ya kwanza ni kwamba alikuwa na mwezi mmoja tu tangu alipoapishwa, “hata Baraza langu la Mawaziri na watendaji wangu nilikuwa sijawateua.”

Mkuu huyo wa nchi alisema kuwa sababu ya pili ilikuwa gharama kubwa za maadhimisho hayo ambazo zilikuwa zimeelekezwa kuwaneemesha wachache.

“Nilipoambiwa gharama za sherehe hiyo mwaka jana zilikuwa bilioni 4 [shilingi]. Nikawa najiuliza hizo bilioni 4 kuna mambo yapi yatakayofanyika? [Wakaniambia] kutakuwa na kualika wageni, kutakuwa na chakula, kutakuwa na posho n.k,” Rais Magufuli alieleza.

“Nilipouliza hizo posho na chakula watakula watanzania wote? Wakasema ni wale wachache tu watakaokuwa wamealikwa. Ndio maana nikaamua kuwa hizo bilioni 4 ziende kupanua barabara la Ali Hassan Mwinyi ambalo linapitiwa na Watanzania wote,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameeleza kuwa shamrashamra za sherehe hizo za Uhuru wa Tanzania Bara zitakuwa za mwisho kufanyika jijini Dar es Salaam na kwamba mwakani zitafanyika Mjini Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi.

Saida Karoli ambariki Darassa kwa ‘Muziki’, amlaumu Mtayarishaji…
Obama atoa amri kuwachunguza Urusi na Trump kuhusu Kilichompiga chini Clinton