Imeeelezwa kuwa, Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli ameteua jopo la wataalam wa maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya tathmini na kuchora ramani ya maendeleo ili aanze kazi tangu siku ya kwanza atakayoingia ikulu.

Hayo yamebainika kupitia taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa umma na kusainiwa na Mjumbe wa kamati ya kampeni, January Makamba. Hata hivyo, taarifa hiyo haikutaja majina ya wataalam wanaounda jopo hilo.

Hivyo ndivyo anavyoeleza:

Maandalizi Ya Kuleta Mabadiliko Ya Haraka Na Ya Kweli

Pia, tunapenda kutoa taarifa kwamba, mgombea wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, ameunda jopo la wanataaluma na wataalamu huru magwiji wazalendo wa uchumi, biashara, utawala na sheria, kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu, asasi zisizo za kiraia, na sekta binafsi, kwa ajili ya maandalizi ya kufanya mabadiliko makubwa Serikalini kuanzia siku ya kwanza atakayokuwa madarakani.

Dkt. Magufuli amelipa jopo hili majukumu yafuatayo:

  1. Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itabana matumizi, ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa;
  2. Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa;
  3. Kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika Serikali;
  4. Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya Serikali inayotekelezwa sasa.
  5. Kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha Sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania;
  6. Kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
  7. Kupendekeza miundo na idadi ya Wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa.
  8. Kupendekeza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wa umma, hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi, ili aanze nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma mabadiliko ya kweli.
  9. Kutengeneza rasimu ya mpango-kazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa kwenye kampeni, hasa upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika;
  10. Kupendekeza muundo wa kitaasisi na utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa nchini.

Dkt. Magufuli ameazimia kuanza kazi mara moja kwa bidii kubwa na maarifa mapya.

 

 

 

Sergio Aguero Nje Mwezi Mmoja
Samatta kuwania Tuzo Ya Afrika