Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ametekeleza agizo la Rais John Magufuli la kusitisha zoezi la ubomoaji wa Hoteli ya Desderia inayomilikiwa na Mbunge Mstaafu wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu).

Zoezi hilo lilikua litekelezwe baada ya Hoteli hiyo kudaiwa kujengwa kwenye chanzo cha maji.

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amenituma nije nikueleze kwamba hakuna mtu yeyote kuja kugusa na kusema anabomoa hoteli hii, kwa sababu huyu ni mwekezaji kama walivyo wawekezaji wengine, na ikiwezekana kama tuna viwanja vingine upande huu wa uzunguni, basi moja kati ya watu ambao wanapaswa kufaidika navyo ni pamoja na sugu,”amesema Chalamila.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea eneo la uwekezaji wa Mbunge huyo na kufikisha agizo la Rais.

“Hoteli hii ilianza kwa kupimwa ardhi, maana yake ardhi hii imepimwa na ina hati. Maana yake watu wa mipango miji na watu wanaohusika na upimaji walishapima,”ameongeza Chalamila.

Kwa upande wake Sugu ambaye ndiye mmiliki wa hoteli hiyo ameshukuru kwa uamuzi huo na kusema anaamini utakuwa chachu kwa wawekezaji wengine.

“Mimi sikuwa na wasiwasi kwa sababu Hoteli haikuota kama Uyoga nilifuata process zote na nashukuru kwa uamuzi huu, naamini itawafanya wengine wafanye uwekezaji kwa kujiamini,” amesema Sugu 

Bilionea wa Urusi afia Zanzibar
Lissu atuma salamu