Rais John Magufuli ameeleza nia yake ya kuboresha mfumo wa elimu nchini kwa kuanza kupambana na ‘wanafunzi hewa’ ikiwa ni siku chache baada ya kuanzisha mapambano dhidi ya wafanyakazi hewa.

Rais Magufuli amewataka watanzania kuacha kuhusisha siasa na masuala nyeti kama ya elimu kwani kwa kufanya hivyo taifa litatengeneza wasomi wa ajabu.

“Nchi yetu ina changamoto na mambo mengi sana hata mimi nimekumbana na changamoto naziona mwenyewe, nikigeuka hivi watumishi hewa ambao hadi sasa wamefikia 10,500, nikigeuka hivi kuna wanafunzi hewa,” Rais Magufuli anakaririwa.

Alisema kuwa kwa kawaida, mwanafunzi wa kidato cha nne aliyefaulu anapaswa kusoma cheti, Stashahada, kabla ya kujiunga na masomo ya shahada chuo kikuu lakini Tanzania imekuwa tofauti na ndio nchi pekee mtu aliyefeli kidato cha nne anaweza kujiunga moja kwa moja na Chuo Kikuu. “Sasa hapa kwetu ni tofauti ukifeli kidato cha nne unajiunga chuo kikuu.”

Rais Magufuli alisema kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakipewa mikopo na Bodi ya Mikopo wakati wanafunzi waliofaulu kutoka kidato cha sita wakiwa wanakosa mikopo hiyo.

Dk. Magufuli ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuivunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) baada ya kubainika kuwa waliridhia wanafunzi wasio na vigezo wenye vyeti vya kidato cha nne kujiunga na Chuo kikuu na kisha kupewa mikopo.

Angalia Orodha Ya Wachezaji 552 Watakaocheza Fainali Za Euro 2016
Unyama: Majambazi yawaua kinyama watu wanane na kuiba sukari, Biskuti