Rais John Magufuli ameagiza uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam kufanyika leo bila kuahirishwa na pasikuwepo kwa maombi ya vizuizi vya mahakama vilivyokuwa vikiwekwa na wanachama wa CCM.

Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ulioahirishwa mara kadhaa kwa sababu mbalimbali huku vurugu kubwa zikizuka ukumbini, unatarajiwa kufanyika leo bila kuahirishwa. Vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vimekuwa vikivutana na CCM.

Akiongea jana Ikulu jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwasilisha silaha zake mbili kwa ajili ya kuhakikiwa, Rais Magufuli aliwataka wanachama wa CCM kutolazimisha kushinda sehemu ambayo hawastahili bali kuhakikisha wanashinda pale wanapostahili.

“Niwaombe wana-CCM wenzangu tusilazimishe mambo. Tukubali kushinda lakini pia tukubali kushindwa. Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli. Lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa… na hiyo ndio demokrasia ya kweli,” alisema Rais Magufuli.

“Tusicheleweshe demokrasia ya wana-Dar es Salaam kwa kila siku kukimbilia mahakamani,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuwa jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika uchaguzi huo.

 

Mwandishi wa ‘DW’ aliyetekwa kabla ya uchaguzi wa Zanzibar asimulia yaliyomsibu
Tanzia: Msafara wa Kamati ya Bunge wapata ajali, watano wafariki