Rais John Magufuli ameahidi kuendeleza kasi ya utendaji wa kazi yake pamoja na operesheni ya kutumbua majipu na kupambana na wala rushwa pamoja na mafisadi.

Rais, Marufuku sukari

Akiongea jana katika hafla fupi ya kuwashukuru makundi mbalimbali ya wasanii na wana habari ambao walimuunga mkono wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, Dk. Magufuli alisema kuwa ndio kwanza ameanza kazi ya kutumbua majipu kwani yapo majipu ambayo ni magumu kupona kwa tiba ya kawaida na kwamba yanahitaji tiba mbadala.

Rais alisema kuwa wale wanaolalamika kufuatia operesheni hiyo  ni bora wakaendelea kulalamika kwani ni zamu yao baada ya Watanzania kulalamika kwa muda mrefu.

“Nitaongeza kasi ya utendaji kazi, wanaolalamika walalamike tu kwa sababu Watanzania wamelalamika kwa miaka mingi, sasa nizamu yao. Ni afadhali watu 1,000 walalamike, lakini Watanzania milioni 50 wafurahie nchi yao. Tukiwaacha wengi hata kwa Mungu tutashindwa kujibu,” alisema Rais Magufuli.

Alieleza kuwa Serikali yake haifanyi operesheni hiyo kwa sababu ya ukatili bali inawalazimu ili mambo yaende vizuri na kwamba katika kipindi chake ni lazima mambo yaende.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alipiga marufuku utoaji wa vibali vya kuingiza sukari nchini kutokana na kuwepo udanganyifu mkubwa wa utoaji leseni unaopelekea kuhujumu viwanda vya sukari nchini.

Rais aliagiza kuwa vibali vyote vya kuingiza sukari nchini visitolewe bila idhini yake kuanzia jana.

Papa Francis, Donald Trump wavutana kuhusu ukristo wa Mgombea huyo
Matokea kidato cha 4: ‘Mchina’ ayeshika nafasi ya pili kitaifa afunika Kiswahili, aliyeongoza aiota Harvard