Hali ya taharuki imetanda nchini Venezuela baada ya chopa (helicopter) ya polisi kushambulia kwa mabomu jengo la mahakama kuu nchini humo hii leo.

Chopa hiyo iliyoangusha mabomu kwenye jengo la mahakama inadaiwa kuibiwa na askari mmoja ambaye bado hajapatikana. Milio ya risasi pia imesikika katika jengo la wizara ya mambo ya ndani.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi, uchunguzi wa awali umebaini kuwepo ujumbe uliotumwa na askari huyo aliyeshambulia jengo hilo, ujumbe unaosomeka “Serikali Ovu”. Shambulio hilo limeripotiwa baada ya kuwepo maandamano ya kupinga hali ya kisiasa na kiuchumi nchini humo.

Vyama vya upinzani vilikuwa vikikosoa vikali utendaji wa mahakama kuu ya Venezuela, ikidaiwa kuipendelea Serikali ya Rais Nicolas Maduro.

Kwa mujibu wa Reuters, hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo ingawa Rais Maduro amesema kuwa tukio hilo alilolitaja kuwa la kigaidi na uasi, lingeweza kuchukua uhai wa makumi ya watu kwani moja kati ya magrunedi yaliyofyatuliwa halikufanikiwa kulipuka.

Rais Maduro ametangaza kuweka jeshi lake katika maeneo yote ya mitaani kulinda nchi hiyo dhidi ya vitendo vya kigaidi.

“Nimeamua jeshi lote la nchi kuingia kulinda amani. Hivi punde au baadae kidogo tutaikamata hiyo helicopter na wote waliohusika katika shambulio hili la kigaidi,” alisema Rais Maduro.

Askari mmoja wa jeshi la polisi ambaye amejitambulisha kwa jina la Oscar Perez, amejitambulisha kupitia mtandao wa Instagram akiwa amezungukwa na watu walioshikilia bunduki wakiwa wameficha nyuso zao kuwa wao ni sehemu ya askari walioamua kupambana dhidi ya kile walichokiita ‘serikali ovu’.

Kitila Mkumbo awapa tano DAWASCO, asema kasi ya utendaji kazi inaridhisha
Wamarekani waupinga mnara wenye amri 10 za Mungu