Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeridhia maombi la Chama Cha Wananchi (CUF) kufungua kesi rasmi dhidi ya Profesa Ibrahim Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

CUF kupitia hati ya maombi iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad waliwasilisha maombi hayo wakiiomba Mahakama Kuu pamoja na mambo mengine kutengua barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Wakili wa CUF, Juma Nassoro amesema kuwa Jaji wa Mahakama hiyo aliyepokea maombi hayo, Jaji Munisi ameridhia na kwamba amewapa siku 14 kuwasilisha maombi rasmi kwa ajili ya kusikilizwa.

“Tumeambiwa tuwasilishe maombi ndani ya siku 14, lakini tutayawasilisha ndani ya siku Saba na tutaiomba mahakakama iyasikilize kwa Hati ya dharula ili shughuli za chama ziendelee,” alisema Wakili Nassoro.

Nassoro alisema kuwa katika maombi hayo pia, wanaiomba Mahakama itoe zuio rasmi kwa Msajili ili asifanye shughuli ambazo ziko nje ya Mamlaka yake aliyopewa na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema kuwa Profesa Lipumba anataka kufungua akaunti nyingine ya chama hicho kwa msaada wa Msajili wa vyama vya siasa ili aweze kuitumia kupokea ruzuku za chama.

Mtatiro amesema kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na amezionya benki zitakazokubali kufungua akaunti hiyo kwani akaunti zote za vyama sharti zifunguliwe kwa ridhaa ya Baraza la Wadhamini lenye wajumbe halali.

Wayne Rooney: Bado Nina Nafasi Ya Kurejesha Makali
Serikali yakanusha kuwepo uhaba wa dawa muhimu