Ikiwa ni saa chache zimesalia kabla Kenya haijafanya uchaguzi mkuu, Mahakama kuu nchini humo imetoa uamuzi juu ya kesi iliyofunguliwa kupinga amri ya wapiga kura kukaa umbali wa mita 400 kutoka katika vituo vya kupigia kura.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Richard Mwongo alisema kuwa sheria inawataka wapiga kura kukaa umbali wa mita 400 kutoka katika kituo cha kupigia kura, ikiwa hawahusiki na zoezi la kuhesabu kura.

Alifafanua kuwa mtu yoyote atakayekaa zaidi ya umbali huo hatapaswi kusumbuliwa tena na vyombo vya ulinzi ikiwa hajihusishi na vitendo vya uvunjifu wa sheria.

Aidha, Mahakama iliitaka Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (IEBC) kuwaruhusu wananchi kuingia katika eneo ambalo kura zimehesabiwa na matokeo yake kusainiwa.

Mlalamikaji aliyefungua kesi hiyo  ya kupinga uamuzi wa IEBC kwa wapiga kura kukaa mita 400 baada ya kupiga kura, Okiya Omtata alisema kuwa uamuzi huo ni kinyume cha Katiba kwani wakenya wanatarajia kupiga kura, kusubiri matokeo kwenye vituo hivyo na kisha kurejea makwao.

Alidai kuwa nyumbani kwake ni umbali chini ya mita 400 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura hivyo sio busara kufikiri kuwa yeye na familia yake wataondoka nyumbani ili wakakae umbali wa mita hizo.

Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu kesho (Agosti 8) ambapo wagombea wanaochuana vikali ni Raila Odinga (NASA) na Rais Uhuru Kenyatta (Jubilee). Kutokana na ushindani mkali unaoshuhudiwa hadi sasa ni vigumu kubashiri nani ataibuka mshindi.

LIVE: Rais Magufuli akihutubia wananchi Handeni, Tanga
Utulivu watawala nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu