Mahakama ya Kuu, kitengo cha Ardhi jana ilitoa maamuzi kuzuia mpango wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutaka kupiga mnada mali za Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kupisha kesi ya msingi iliyofunguliwa mahakamani hapo.

Mbowe alifungua kesi ya kupinga uamuzi wa NHC kumuondoa katika jengo lililopo katikati ya jiji la Dar es Salaam lililokuwa na biashara ya club Bilcanas na gazeti la Tanzania Daima, pamoja na kutaka kupiga mnada vitu vyake vilivyokuwa kwenye jengo hilo.

Katika shauri hilo lililofunguliwa mahakamani hapo na Mbowe akiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala na mwenzake, mlalamikaji anapinga kudaiwa shilingi bilioni 1 na shirika hilo la nyumba.

Akisoma uamuzi wa Mahakama hiyo, Jaji Siyovelwa Mwangasi alisema kuwa anakubaliana na maombi ya upande wa mlalamikaji na kuitaka NHC kusitisha mpango wake wa kupiga mnada mali za mlalamikaji.

Mbowe amekuwa akipinga kudaiwa na NHC ‘hata senti moja’ huku akidai kuwa yeye pia ni mmiliki wa jengo hilo kwani alinunua asilimia 75 ya hisa za jengo hilo tangu mwaka 1997.

Hoja hizo za Mbowe zilipingwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyeeleza kuwa anachofahamu ni kwamba NHC haina ubia na mtu yeyote katika umiliki wa jengo hilo.

Serikali kununua gari ya wagonjwa yenye dhamani ya sh. mil. 200 hospitali ya Muheza, Tanga
Lipumba amvaa Lowassa, adai hatakubali ainunue CUF bei chee