Mahakama Kuu ya Gauteng Johannesburg nchini Afrika Kusini imeamuru kuachiwa huru kwa ndege ya Airbus ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oliver Tambo.

Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilizuiwa katika uwanja huo Agosti 23, 2019 kwa amri ya mahakama hiyo baada ya Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya dolla milioni 33.

Taarifa hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwele mara baada ya uzinduzi wa mkutano wa wadau wa sekta ya ujenzi Tanzania ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa mgeni rasimi.

Amesema kuwa kwasasa ndege hiyo imeachiwa huru kuendelea na safari zake, hivyo amewataka Watanzania kutokuwa na hofu yeyote kuhusu ndege hiyo.

”Kwasasa ndege yetu iko huru kuendelea na safari zake kutoka Afrika Kusini, hivyo Watanzania wasiwe na wasi wasi wowote katika hilo, kwasasa limekwisha,”amesema Waziri Kamwelwe

Kwa upande wake msemaji mkuu wa serikali, Dkt. Hassan Abbas kupitia akaunti yake ya Twitter ameandika kuwa, ”Mahakama Kuu ya Gauteng ya Afrika Kusini imetoa hukumu na kuamuru ndege hiyo iachiwe huru”

JPM awataja Makamba na Ngeleja, 'Niliamua kuwasamehe'
Lissu azungumzia tarehe ya kurudi Tanzania