Nahodha wa timu ya taifa ya Peru Paolo Guerrero, huenda akacheza fainali za kombe la dunia, kufuatia amri ya mahakama ya usuluhishi ya nchini Uswiz ya kumuondolea adhabu ya kufungiwa kucheza soka kwa miezi 14, iliyotangazwa na mahakama ya usuluhushi wa michezo duniani (CAS) mwezi uliopita.

Mahakama hiyo imefikia maamuzi hayo, baada ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, kukata rufaa ya kupinga maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yake, ya kufungiwa kucheza soka kwa muda wa miezi 14.

Maamuzi ya mahakama ya usuluhisi ya Uswiz yameeleza kuwa, vilelezo vilivyotumika kumfungia Guerrero havikua na uthibitisho uliotosha, hivyo anapaswa kuachwa huru na kushiriki fainali za kombe la dunia.

Guerrero alibainika kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni, baada ya kupimwa mwezi Oktoba mwaka jana, katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Argentina.

Wakala wa kupinga matumizi ya dawa za kulevya michezoni (WADA), walithibitisha taarifa hizo na kuwaziwasilisha FIFA, kabla ya maamuzi ya kufungiwa kucheza soka kwa miezi 12 kutolewa.

Guerreo alikata rufaa CAS kupinga adhabu hiyo, kwa kuwasilisha utetezi wa kuhisi huenda alikutwa na maswahibu hayo baada ya kunywa chai yenye viungo saa chache kabla ya mchezo dhidi ya Argentina, lakini bado ilithibitika alitumia dawa hizo kwa makusudi, na aliongezewa kifungo hadi kufikia miezi 14.

Peru wamepangwa katika kundi C lenye timu za Australia, Denmark na Ufaransa.

Peru walijihakikishia ushiriki wa fainali za kombe la dunia mwaka huu, baada ya kuifunga New Zealand katika mchezo wa mtoano mwezi Novemba 2017.

Kwa mara ya mwisho Peru walishiriki kwenye fainali hizo mwaka 1982.

Mrithi wa Zidane bado kitendawili Real Madrid
Video: Tazama Diamond akifunga ndoa na Zari ndani ya 'Iyena'