Mahakama Wilaya ya Ilala, imeamuru kampuni ya MIC Tanzania (Tigo) kuwalipa wasanii wa Bongo Flava, Ambwene Yesaya maarufu kama AY na Hamisi Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, kiasi cha shilingi bilioni 2, kwa kutumia nyimbo zao bila idhini.

Tigo walibainika kutumia nyimbo za wasanii hao kwa kipindi tofautia kama miito ya wateja wao na kufanya biashara bila idhini ya wasanii husika.

Hakimu Mkazi Mwanadamizi wa Mahakama ya Ilala, Juma Hassan alitoa hukumu hiyo Aprili 11 mwaka huu, baada ya kuendeshwa kwa kesi hiyo kwa kipindi cha miaka minne. Mbali na shilingi bilioni 2, Tigo waliamriwa kuwalipa wasanii hao shilingi milioni 25 kama damages.

Taarifa za uamuzi wa mahakama ya Ilala zimebainika wiki hii baada ya Tigo kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Mwana FA aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi wa Mahakama ya Ilala ni kitu ambacho kilipaswa kutokea tangu zamani katika tasnia ya muziki ili wasanii wapate haki zao.

“Hiki ni kipindi muhimu kwa Haki Miliki hapa Tanzania,” alisema Mwana FA. Hiki ni kitu ambacho kilikuwa kikifanyika kwa miaka mingi kutokana na kukosekana kwa uelewa na labda gharama za endeshaji wa kesi kama hizo,” alisema Mwana FA.

“Hakuna mtu mwenye haki ya kutumia kazi yako bila ruhusa yako au makubaliano. Na kama amefaidika anapaswa kugawana na wewe kutokana na bei uliyojiwekea kwenye kazi yako,” aliongeza rapa huyo.

Nyimbo ambazo zinadaiwa kutumiwa na Tigo bila idhini ya wasanii hao ni ‘Dakika Moja’ na ‘Usije Mjini’ ambazo zote wamefanya kwa pamoja.

Kesi hiyo ya rufaa imeahirishwa hadi itakaposikilizwa tena kesho katika Mahakama Kuu.

The Merengues Waendelea Kutesa kwa Utajiri Duniani
Ibrahim Ajib Aikana Simba Iliyomfikisha Alipo Sasa