Serikali nchini Uganda leo imeshinda kesi iliyofunguliwa na upande wa upinzani kupinga mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa umri wa kugombea nafasi ya urais.

Mahakama ya Juu nchini humo imebariki uamuzi uliotolewa awali na Mahakama ya Katiba wa kuondoa ukomo wa umri wa mgombea urais, hatua ambayo imetafsiriwa kuwa ni kumpa uhalali Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 74 kugombea tenda urais mwaka 2021.

Akisoma uamuzi wa jopo la majaji saba, Jaji Mkuu Bart Katureebe amesema kuwa rufaa iliyokatwa imeshindwa kwakuwa majaji wanne kati ya saba wameitupilia mbali.

Rais Museveni amekuwa madarakani tangu mwaka 1986. Disemba mwaka jana alisaini muswada wa kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais uliopitishwa na Bunge la nchi hiyo ukiungwa mkono na wabunge wa chama tawala walio wengi, huku kukiwa na pingamizi kutoka kwa upande wa upinzani.

Wapinzani wamekuwa wakidai kuwa hatua hiyo inamfanya Rais Museveni kuwa kiongozi wa maisha wa nchi hiyo. Awali, Katiba ya nchi hiyo ilikuwa imeweka umri wa miaka 75 kuwa ndio ukomo wa umri wa mgombea Urais. Kwa jinsi ilivyokuwa, Museveni asingeweza kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.

Nicki Minaj aitosa menejimenti yake
Kanisa laanguka, 13 wapoteza maisha