Mahakama ya Kikatiba nchini Jamhuri ya Kidekrasia ya Congo (DRC), imetupilia mbali maombi ya kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 30, yaliyomtaja Felix Tshisekedi kama mshindi wa Urais.

Mahakama hiyo imeeeleza kuwa hakuna ushahidi usio na shaka uliowasilishwa na upande wa mlalamikaji, Martin Fayulu ulioushawishi kuyafuta matokeo hayo.

Martin Fayulu akiwa Mahakamani na jopo la mawakili pamoja na timu yake

Fayulu amedai kuwa yeye ndiye mshindi wa uchaguzi huo na kwamba Tshisekedi aliingia makubaliano maalum na Rais Joseph Kabila na kusababisha matokeo hayo kubadilishwa, madai ambayo timu ya Tshisekedi imeyakanusha vikali.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) ilimtangaza Tshisekedi akiwa na kura milioni 7 (38.5%), dhidi ya mpinzani wake Fayulu aliyekuwa na kura milioni 6.4 (34.7%) huku mgombea wa chama tawala, Emmanuel Shadary akiambulia takribani kura Milioni 4 (23.8%).

Aidha, Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo ambalo lilisambaza waangalizi 40,000 kwenye vituo vya kupigia kura limedai kuwa linayafahamu matokeo halisi na kwamba matokeo ya CENI hayaendani na takwimu walizokusanya.

Ingawa Mahakama imeyabariki matokeo ya CENI ikiwa ni siku tano tu kabla ya kumuapisha Rais Mteule Tshisekedi kuwa Rais wa DRC, Fayulu ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa yeye ndiye mshindi.

Ameitaka Jumuiya ya Umoja wa Mataifa pia kutoyatambua katokeo ya CENI kama matokeo halali na rasmi ya uchaguzi wa Desemba 30 mwaka jana.

Serikali ya Marekani, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameonesha shaka kuhusu matokeo yaliyotangazwa na wametaka matokeo hayo kupitiwa upya.

Simba yaufyata kwa AS Vita, yapokea kipigo cha 'Mbwa koko'
Makala: Lowassa au Lissu, nani agombee urais 2020?