Mahakama ya Katiba nchini Cameroon imetupilia mbali maombi 18 ya pingamizi la matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo yaliyowasilishwa na ngome ya upinzani.

Katika mapingamizi hayo, wapinzani waliiomba mahakama hiyo kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 7 na kuitisha uchaguzi mwingine kwa madai kuwa haukuwa huru na haki.

Uamuzi huo wa mahakama unatoa baraka kwa Tume ya Uchaguzi kumthibitisha Rais Paul Biya kuwa mshindi wa uchaguzi huo muda wowote kabla ya Jumapili wiki hii.

Rais Biya mwenye umri wa miaka 85 ameitawala nchi hiyo ya Afrika ya Kati kwa miaka 36.

Rais wa Cameroon, Paul Biya (mbele)

Uchaguzi wa nchi hiyo ulifanyika wakati ambapo kulikuwa na mvutano ulioibuliwa tangu mwaka 2016 katika maeneo ya Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi mwa nchi hiyo, na jamii ya watu wanaozungumza lugha ya kiingereza (Aglophone).

Katika kipindi hicho, walimu pamoja na wanasheria wa jamii ya wanaozungumza Kiingereza waliingia mitaani kufanya maandamano makubwa kupinga uamuzi wa matumizi ya Kifaransa mashuleni na mahakamani.

Aidha, harakati hizo zilitanuka na kuchukua mkondo wa kisiasa ambapo maelfu ya watu waliingia mtaani Oktoba Mosi mwaka jana wakijitangazia uhuru wao kwa madai kuwa wana nchi mpya inayoitwa ‘Ambazonia’.

Hata hivyo, Serikali ilifanikiwa kuzima harakati hizo, huku wananchi takribani 420 na wanajeshi 175 wakiripotiwa kupoteza maisha.

International Crisis Group imeripoti kuwa zaidi ya watu 300,000 walilazimika kuyahama makazi yao kufuatia vurugu hizo.

Waziri apinga ushauri wa watu kupunguza ulaji wa nyama
Polisi waingilia kati mafuriko ya watu soko 'halali' la bangi

Comments

comments