Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma leo imekubaliana na uamuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumvua ubunge, Joshua Nassari.

Akisoma uamuzi wa Mahakama leo, Jaji Latifa Mansour ameeleza kuridhishwa na hoja za upande wa Serikali kuhusu uamuzi huo kwani Nassari alikosa sifa za kuendelea kuwa Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa mujibu wa sheria.

Spika Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kumueleza kuwa jimbo hilo liko wazi hivyo atangaze uchaguzi mwingine kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Akizungumzia uamuzi wake, Spika Ndugai alisema kuwa Nassari hakuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge bila ruhusa, hivyo kukosa nafasi ya kuendelea kuwa mbunge kwa mujibu wa sheria. Aliitaja mikutano hiyo kuwa ni wa Septemba, Novemba na wa Januari mwaka huu.

Awali, Nassari alieleza kuwa aliandika barua na kuituma kwa njia ya barua pepe baada ya kuwasiliana na msaidizi wa Spika Ndugai, lakini Spika alieleza kuwa hakuwahi kupata barua yake zaidi ya kuiona nakala aliyoweka mtandaoni. Alisema kuwa alikuwa nje ya nchi akimuuguza mke wake ambaye anasumbuliwa na matatizo ya uzazi.

Aidha, Jaji Mansour ameeleza kuwa Nassari alikosea katika kufuata taratibu, na kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 5 (4) alipaswa kupeleka malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge.

Nassari amekuwa mbunge wa kwanza wa upinzani katika bunge la 2015-20 kuvuliwa ubunge kwa sababu za kutohudhuria mikutano ya bunge hila ruhusa.  Mbunge huyo wa Chadema alikuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2012, ambapo alichaguliwa tena mwaka 2015.

Hatutamfukuza mbunge yeyote CUF- Khalifa
Video: Wasanii Morogoro wapelekewa mikopo hadi mlangoni, Kopafasta wamtambulisha Wakala