Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imewatoa hofu wananchi wanaofuatilia kesi ya kupinga matokeo ya Ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na David Kafulila (NCCR-Mageuzi) dhidi ya Hasna Mwilima (CCM), baada ya kushindwa kuanza kusikilizwa jana.

Mahakama hiyo ilishindwa kuanza kusikiliza kesi hiyo jana kama ilivyokuwa imepangwa baada ya mlalamikiwa, Mwilima pamoja na wakili wa Serikali kutofika mahakamani huku upande wa mlalamikaji ukihudhuria.

Kufuatia hatua hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Sylvester Kainda alitoa taarifa kwa niaba ya Jaji Ferdinand Wambali kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa tena Machi 9, 2016 na kuwaomba mamia ya wananchi waliokuwa wamehudhuria kutokuwa na hofu.

Alisema kuwa kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa haitasimama hadi itakapomalizika na uamuzi wa Mahakama kujulikana.

“Kesi itakapoanza kusikilizwa Machi 9 mwaka huu itaendelea bila kusimama hadi itakapomalizika. Huo ndio msimamo wa Jaji wa Mahakama Kuu, baada ya kukaa na wahusika. Hivyo, wananchi wasiwe na hofu yoyote,” Hakimu Kainda.

Wakili wa Kafulila katika kesi hiyo ni Profesa Abdallah Safari, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

TFF, KTA Zazindua Programu Ya Maendeleo Ya Soka Kwa Wanawake
Sekta ya afya kupewa bei elekezi, Mlima wawekwa Kuingia Muhimbili