Mahakama Kuu Kanda ya Ziwa imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na Mwanasheria Mkuu kuhusu shauri lililofunguliwa mahakamani hapo na baba mdogo wa marehemu Alphonce Mawazo, ndugu Charles Lugiko akisaidiwa na mawakili watatu wa Chadema.

Katika pingamizi hilo, Kamanda wa Polisi na mwanasheria mkuu waliitaka mahakama kufuta kesi namba 10 mwaka 2015 iliyofunguliwa kudai kuuaga mwili wa Mawazo jijini Mwanza na kwa madai kuwa mfungua shtaka hana uhalali wa kuwasilisha maombi hayo kwa kuwa yeye siyo baba mzazi wa marehemu.

Jaji wa mahakama Kuu anayesikiliza shauri hilo, Lameck Mlacha alieleza kuwa hoja za mawakili wa serikali hazikuwa na mashiko kwa kuwa mtoa maombi alimlea marehemu tangu akiwa na umri wa miezi miwili, hivyo ana uhalali wa kufungua shauri hilo.

Hivyo, Jaji Mlacha aliamua kuwa shauri la msingi lililofunguliwa dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali na kamanda wa polisi litasikilizwa leo chini ya hati ya dharura sana.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza furaha yake juu ya uamuzi uliotolewa na kuongeza kuwa wanasheria wa chama hicho wataendelea na taratibu za kudai haki ya kuaga mwili wa mawazo katika jiji la Mwanza kabla ya kumpumzisha mkoani Geita.

“Tumepokea vyema sana maamuzi ya Jaji kwamba mapingamizi yaliyofunguliwa na Serikali hayana mashiko na kutoa ruhusa sasa kwa mawakili wa upande wa walalamikaji kuleta rasmi hati ya malakamiko,” alisema Mbowe.

Alphonce Mawazo aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Geita, aliuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga mkoani Geita.

 

 

Picha: Wakimbizi wajishona midomo kwa uzi kupinga katazo la kuvuka mpaka
Waziri Mkuu aanza na Mkwamo wa Mabasi ya Mwendo Kasi, atoa Saa chache kupewa majibu