Mahakama nchini Kenya imewaachia huru watuhumiwa watatu wa shambulizi la kigaidi kwenye jengo la 14 Riverside Dusit Complex jijini Nairobi nchini Kenya.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Polisi kupitia Kitengo Maalum cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) kuwaondolea mashtaka watuhumiwa hao kutokana na upelelezi wa awali.

ATPU imeiambia Mahakama kuwa wamebaini watuhumiwa Abdul Kibiringi, James Mwai Mwangi na Habiba Gedi Hunshur hawakuhusika kwa namna yoyote kufanikisha tukio hilo.

Kwa mujibu wa Standard Media, Kamanda wa Polisi, Gitonga Muthoga anayeshughulikia masuala ya kihalifu kwenye kitengo hicho, amesema wanafuatilia kwa ukaribu mienendo ya watuhumiwa pamoja na maendeleo ya kesi dhidi yao mahakamani.

Amesema kuwa kitengo hicho kimempeleka kwenye tiba maalum (rehabilitation) mtuhumiwa mmoja ambaye amebainika kuwa ameharibiwa kisaikolojia kuamini katika ugaidi.

Watuhumiwa kadhaa wa ugaidi wameendelea kusota rumande huku watuhumiwa wengine walionaswa wakiwasiliana na magaidi waliofanya mashambulizi hayo wakiendelea kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kundi la A-Shabaab lilitekeleza mashambulizi ya kigaidi Januari 15 mwaka huu jijini Nairobi na kusababisha vifo vya watu 21.

Jeshi la Kenya kwa kushirikiana na Vikosi vya Umoja wa Mataifa limeendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Al-Shabaab nchini Somalia kwa lengo la kulitokomeza.

Kagame awa mwenyekiti EAC, aeleza atakachofanya
Sakata la CAG, Spika Ndugai Mahakama yatoa uamuzi