Mahakama nchini Tanzania zimeokoa fedha za kitanzania milioni 129 baada ya kuendesha vikao kwa njia ya mtandao (video conference) 2019.

Kati ya fedha hizo, Mahakama ya Rufani Tanzania, imefanikiwa kuokoa milioni 95 katika kipindi cha oktoba 2019 baada ya kuendesha vikao maalumu kwa njia ya mtandao wakati Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ikiokoa milioni 34 katika kipindi cha mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuhusu maadhimisho ya wiki ya utoaji wa elimu ya sheria na siku ya sheria nchini, jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma amesema katika kipindi cha mwaka jana Mahakama ya rufani iliendesha vikao hivyo ambavyo vilifanyika kwa njia ya video conferencing kwenye vituo vya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya, Tabora na Bukoba.

Amesema jumla ya maombi 60 yalisikilizwa na majaji 18 wa Mahakama hiyo ambapo kila Jaji alipangiwa kusikiliza maombi kati ya mawili na sita,

“Gharama za zoezi zima la kutumia video conferencing ilikuwa milioni 5 ambayo ilihusisha gharama za internet, pamoja na usafiri wa watumishi kwaajili ya kwenda kuratibu zoezi hilo”

“Gharama hizo zilijumuisha pia kuwalipa mawakili wa kujitegemea wanaotakiwa kuwawakilisha wafungwa walio magerezani kwa makosa ya mauaji” Amesema Jaji Mkuu.

Amefafanua kuwa kutokana na kutumika kwa njia hiyo, majaji walibaki Jijini Dar es salaam lakini waliweza kusikiliza maombi na kisha kurudi maofisini kuendelea na shughuli zao nyingine.

Mvua kubwa kunyesha mikoa ya kanda ya ziwa, TMA yatoa tahadhari
Live: Maswali na majibu Bungeni leo Januari 29