Waziri wa afya nchini Kenya Cleophas Mailu ametaka uchunguzi wa kina kufanyika katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta baada ya wanawake waliojifungua katika hospitali  hiyo kudai wanadhalilishwa kingono.

Taarifa zilizoenea ni kwamba kina mama wanaojifungua wamekuwa wakishambuliwa kwa kudhalilishwa kingono na baadhi ya wafanyakazi wakati wakienda kwenye chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook ulianza kuibua mkasa huo, ambapo kulikuwa na ujumbe ulioandikwa katika ukurasa wa Buyer Beware ambao mara nyingi hutumiwa kuwatahadharisha wateja na wanunuzi wa bidhaa na huduma.

Ujumbe huo umewatahadharisha kina mama wanaojifungulia katika hospitali hiyo kwamba wamo hatarini kudhalilishwa kingono na baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo.

Hata hivyo wanawake wengine waliowahi kupatiwa huduma katika hospitali hiyo wamedhihilisha kutokea kwa udhalilishaji huo katika hospitali hiyo na kudai wamewahi kudhalilishwa.

Aidha Waziri Mailu ameagiza uchunguzi wa dharura kufanyika na ripoti kamili kuwasilishwa kwake kufikia Jumatatu

Wasimamizi wa hospitali hiyo wamesema hawajapokea malalamiko yoyote.

Afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo Lily Koros amesema hakuna mwanamke hata mmoja aliyewahi kulalamika kwamba alidhalilishwa kingono hospitalini humo.

Amesema hospitali hiyo huwa chini ya uangalizi wa kamera za usalama (CCTV) wakati wowote na hakuna kisa hata kimoja kilichogunduliwa.

Mpina awataka wafugaji kupaza sauti
Majaliwa amsweka ndani Mkurugenzi