Majaji wa Mahakama ya Kuu na Mahakama ya Katiba nchini Uganda wamelalama kuhusu mishahara midogo, mazingira ya kazi yasiyoridhisha na idadi ndogo ya watendaji.

Akizungumza wiki hii jijini Kampala mbele ya Rais Yoweri Museveni, katika uzinduzi wa Mkutano wa  21 wa Mwaka wa Kimahakama, Jaji wa Mahakama ya Katiba, Hellen Obura alimuomba Rais kuwaongezea mishahara na kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi katika chombo hicho cha kutoa haki.

Jaji Obura alisema kuwa kukosekana kwa rasilimali za kufanikisha utendaji kikamilifu ni tishio kubwa dhidi ya utendaji wenye ufanisi.

Aidha, alimuomba Rais Museveni kuwasaidia kuinua kipato chao ili waweze kumudu ipasavyo gharama za maisha na kuondokana na misongo ya mawazo inayotokana na vipato visivyokidhi gharama za maisha.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akisaini bango la Mkutano wa 21 wa Kimahakama

Kwa mujibu wa Uganda Press Review, Jaji huyo pia alimuomba Rais kuielekeza Wizara ya Fedha kutoa fedha za fungu lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia Mahakama. Alieleza kuwa endapo fedha hizo zitatolewa kwa muda zitasaidia kuongeza idadi ya majaji hadi 82.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu, Justice Bart Katureebe alimuomba mkuu huyo wa nchi kuondoa katazo la kutoajiri mahakimu wapya na akasisitiza ombi la kuongezwa kwa idadi ya majaji hasa wa Mahakama ya Rufaa.

Hata hivyo, akijibu maombi yaliyowasilishwa kwake, Rais Museveni alilikataa ombi la kuongeza idadi ya Mahakimu.

“Kwa sababu, kama hamuwezi kuweka kipaumbele cha kimkakati mtashindwa, kama hamtaweka kipaumbele ndani ya sekta mtashindwa kwa sababu hamna rasilimali za kutosha,” alisema Museveni.

“Kwahiyo, badala ya kusisitiza katika kuongeza idadi zaidi, wakati hamuwezi kuwasimamia ipasavyo. Ningejikita zaidi katika kuwaboreshea mishahara waliopo halafu tuone ni jinsi gani tunaweza kushughulikia tatizo la upungufu,” aliongeza.

Museveni aliwahakikishia kuwa atalifanyia kazi suala la kuboresha mishahara na mazingira ya kazi kuliko kujikita katika kuongeza idadi.

Video: Msichana aliyeongoza kidato cha 4 asimulia alivyowahi kuanguka
Video:Ndoto za wazazi zapelekea Mariam kuongoza kitaifa

Comments

comments