Waziri Mbuu, Kassim Majaliwa amewaagiza mkuu wa wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Shaib Nnunduma pamoja na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Eric Mapunda kuimarisha doria kwenye eneo la bahari ili kuzuia uvuvi haramu.

Majaliwa amesema vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea katika wilaya hiyo vinapaswa kudhibitiwa haraka kwa sababu vinasababisha halmashauri hiyo kukosa mapato na kushindwa kuboresha maendeleo ya wananchi.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu kwa nyakati tofauti Septemba 24, 2016 wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Tanpesca na alipowahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kirongwe wilaya ya Mafia.

Majaliwa amesema uvuvi ndiyo shughuli kuu ya uchumi na chanzo muhimu cha mapato kwa wilaya ya Mafia na suala la uvuvi haramu linaathiri sana mapato ya halmashauri hivyo ni vema wakaimarisha doria ili kukomesha vitendo hivyo.

Amesema uvuvi wa kutumia mabomu unaharibu mazingira ya chini ya bahari hivyo samaki wanashindwa kuzaliana kwa wingi.

“Hakikisheni watu hao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuteketeza zana wanazotumia”. – Majaliwa

Rais Magufuli awashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa
Viongozi wa Vyama vya Siasa Watakiwa kuwa wazalendo