Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameonyesha kushangazwa na kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo Dodoma hali iliyopelekea kuliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma kufanye marekebisho ya kodi hiyo ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.

Majaliwa amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.

Majaliwa ametoa agizo hilo Oktoba Mosi, 2016 wakati alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Majaliwa amesema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.

Amesema kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na baraza la Madiwani, hataki kuvunja sheria, anawaagiza wazungumze tena katika baraza na kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo.

Majaliwa amesema hali hiyo haiwezi kuachwa iendelee, kwani inawaumiza wananchi.

“Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” – Majaliwa.

Manispaa hiyo imetakiwa kuhakikisha makusanyo yote ya fedha katika soko hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua wotewatakaobainika kuiba fedha hizo.

Majaliwa pia ameiagiza Manispaa hiyo kupanua masoko kwa kujenga masoko mapya makubwa katika maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili huduma hizo zisambazwe.

Akisoma risala, Mwenyekiti wa soko hilo, Godson Rugazama alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo kuwa ni pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli za wajasiriamali sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi 150,000 kwa mwezi,” alisema.

Mwenyekiti huyo ametaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyokuwa rasmi na kusababisha wateja kutoingia sokoni.

 

Waziri wa afya aagizwa kuimarisha hospitali ya Dodoma
Video: RC Makonda atangaza adhabu kwa waharibifu wa mazingira Dar