Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Amesema kuwa Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika shughuli nyingine jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere.

Aidha, Majaliwa pia ameagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama, Solomon Ngiliule pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri, Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri  hiyo. Robert Makendo.

Hata hivyo ameongeza kuwa viongozi hao wanatakiwa wachunguzwe kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwemo sh. milioni 12 walizotumia kuandaa profile ya Halmashauri hiyo.

Katika hatua nyingine, Majaliwa aliiagiza Taasisi ya Kuzuzia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) mkoani Mara imkamate na kumuhoji Meneja wa Wakala wa Majengo  Tanzania (TBA) mkoani Mara, Mhandisi Peter Salim  baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

 

Dkt. Mwakyembe awasihi Watanzania kumsaidia Wastara
Ubadhirifu mkubwa wabainika Shirika la Posta