Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa viwanda vikubwa viwili vya kuchakata pamba ambao wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu huu.

Viongozi hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi na Mkurugenzi Mtendaji wa JOC Bw. Qin Mengwei ambao kwa pamoja wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa.

Amekutana na viongozi hao hii leo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa wakulima waliitikia wito wa Serikali wa kufufua zao hilo, hivyo mwaka huu wanatarajia kupata mavuno mengi.

Aidha, amewataka viongozi hao wajiandae kununua pamba nyingi kwa sababu mwaka huu wakulima wamelima pamba ya kutosha baada ya Serikali kuwahamasisha waongeze uzalishaji kwa kuwa kuna soko la uhakika.

“Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa hiyo tarehe 21, Februari, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua mbegu za pamba, ili mradi wanajihusisha na pamba nanyi naomba muwepo,”amesema Majaliwa

Kwa upande wao, Bw. Pardesi na Bw. Qin wamemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kampuni zao zinauwezo wa kununua pamba yote inayozalishwa nchini na kuichakata katika viwanda vyao na kutengeneza nyuzi na nguo zitakazouzwa nchini kwa bei nafuu.

Rais afanya uteuzi mwingine
Video: Hakuna maisha magumu kama kuishi kinafiki- Bashe