Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali ipo makini na ajira za wageni na itaendelea kuhakikisha kuwa watanzania wanapewa fursa kwanza.

Ameyasema hayo hii leo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Leah Komanya aliyetaka kupata kauli ya serikali juu ya wageni wanaoingia nchini na kupata ajira kwenye maeneo nyeti kama vile bandarini au viwanja vya ndege.

“Ajira zote za wageni nchini Tanzania ni kwa nafasi zile za kitaalam tu ambazo Watanzania hawana uwezo nazo na hatujaacha wazi, tumeweka ukomo kuwa ni wageni watano tu kwa kila taasisi ndio wanapata fursa ya kuajiriwa ndani ya nchi, kuitumikia taasisi hiyo na ni kwa nafasi ambazo watanzania hawana uwezo nazo,”amesema Majaliwa

Amesema kuwa pale ambapo italazimu raia wa nje apate ajira, serikali itaendelea kusimamia ili kuhakikisha kama kweli nafasi hiyo haina mtu na ni nafasi nyeti yenye utaalam ambao hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.

Hata hivyo, Majaliwa amesema endapo atakutwa mtu yeyote wa Taifa la nje anafanya kazi kwenye maeneo hayo, basi atakuwa ameajiriwa na kampuni ambayo inafanya shughuli maalum kwenye eneo hilo na kwa masharti yale yale kwamba watapata nafasi kufanya kazi kwenye kampuni hiyo kama nafasi hiyo hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.

 

Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Mei 18, 2018
TRA yamlima notisi ya siku 30 Makonda