Waziri Mkuu, Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, kwa kuwawezesha wanawake walioajiriwa ndani ya kampuni hiyo kujiendeleza kielimu pamoja na kuwapa promosheni za nafasi mbalimbali ikiwemo za uongozi pindi wanapohitimu mafunzo au masomo yao.

Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Tanzania), iliyoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania – ATE, ambapo jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti wakiwamo wahitimu wanne kutoka GGML.

Amesema; “Nimefurahi kusikia wanawake kadhaa waliohitimu katika program hii wamefanikiwa kupata nafasi za juu za uongozi kama dada yetu wa GGML (Tatu Tibashengwa), hayo ndio mafanikio tunayoyataka.”

Aidha, Majaliwa pia aliwataka wanawake wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali huku Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Doran akisema kuwa tangu waanze programu hiyo kwa kushirikiana na ESAMI, wametoa mafunzo kwa wanawake 274 kutoka kampuni 79 wakiwemo Wabunge na wawakilishi 150.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya GGML, Terry Strong, Kaimu Meneja Rasilimali Watu, Dominic Marandu alisema tangu mafunzo hayo yalipoanzishwa mwaka 2016, GGML imepeleka jumla ya wafanyakazi wa kike 17 katika program ya kuwapatia mafunzo hayo ya Female Future Tanzania – FFT.

Alisema “hivi sasa tupo katika mchakato wa kupendekeza majina ya wafanyakazi wengine wanne wa kike katika program inayofuatia,” alisema. Alisema GGML itaendelea kuongeza ujumuishwaji, usawa na kukubaliana na tofauti mbalimbali zilizopo katika makundi ya kijamii.

Akizungumzia promosheni aliyoipata kutoka GGML, Tatu Tibashengwa mbali na kueleza kuipokea kwa furaha, aliishukuru kampuni hiyo kwa kutambua utendaji wake uliotukuka, ufanisi, ujasiri na hata kudumisha dhana ya usawa wa kijinsia mahala pa kazi.

TANAPA yaweka mikakati kumaliza migogoro maeneo ya Hifadhi
Kuuza figo ni kosa kisheria: Dkt. Chandika