Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Uingereza kuhamasisha wawekezaji zaidi kutoka nchini humo kuja kuwekeza kwenye sekta ya viwanda hapa nchini.

Majaliwa hayo leo Jumanne, Novemba 8, 2016 wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke alipomtembelea ofisini kwake Bungeni, mjini Dodoma, ambapo amemuomba kualika wawekezaji wengi zaidi kwenye maeneo ya kilimo, viwanda vya usindikaji mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji, sekta ya mafuta na gesi, nishati na ujenzi wa makazi hasa kwa mkoa wa Dodoma ambako hivi sasa ni Makao Makuu ya Serikali.

Majaliwa amesema kuwa Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati na hivyo imejipanga kuwa na viwanda vya kutosha ili iweze kusindika mazao yake hapa nchini na itoe ajira kwa wananchi wake,pia ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa msaada wake mkubwa wa ujenzi wa nyumba za walimu na shule mkoani Kagera zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.

Kwa upande wake Cooke, amesema ameguswa na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na masuala ya ufisadi na rushwa. “Kaulimbiu yenu kwamba rushwa haikubaliki (zero tolerance on corruption) inaonyesha jinsi mlivyodhamiria kupambana na baa hili” alisema.

Ameongeza kuwa Uingereza inaongoza miongoni mwa nchi zenye wawekezaji wengi hapa nchini na kwamba inaendeleza mpango wake wa uwekezaji ambao unalenga maeneo makuu manne ambayo ni gesi na mafuta; kilimo; nishati jadidifu na uimarishwaji wa mazingira ya kufanya biashara.

Aidha, Cooke ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa Serikali kutokana na msiba wa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo, Tabora,  Samuel Sitta kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 7, 2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu.

 

Ali Kiba ataka MTV EMA kueleza kwanini hawakumpa tuzo iliyoenda kwa Wizkid
Tanzia: Mungai afariki Dunia