Serikali imewataka wananchi kuchukua tahadhari na hatua stahiki za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kubadili mwenendo wa ulaji usiofaa kutokana na magonjwa hayo kuchangia vifo zaidi ya milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016 ulimwenguni.

Wito huo umtolewa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa jijini Dodoma Novemba 14, 2019 wakati akizindua wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na kudai kuwa takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuitaka jamii kula mboga mboga, matunda na kufanya mazoezi.

Amesema kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe na kutoa hamasa kwa jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu ikiwemo kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza viungo vya chumvi, sukari na mafuta.

“Magonjwa yasiyoambukizwa yanakua tishio kwa afya zetu hivyo tujipange kukabiliana nayo maana yana madhara makubwa ingawa kuna uwezekano wa kuyadhibiti tupunguze ulaji usiofaa na tuongeze bidii ya vyakula vya mboga mboga na matunda,” amefafanua Waziri mkuu.

Aidha Waziri Mkuu ameongeza kuwa wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki na kwamba inawapasa kukabiliana na magonjwa mengine kama inavyoelekezwa na wizara ya afya kupitia mpango huo.

Kuhusu mkazo katika suala la afya Waziri mkuu ameweka msisitizo kwa sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na Makamu wa Rais Samia Suluh Hassan kwani utaratibu huo utasaidia kuboresha afya za wananchi.

“Niseme tuendelee kuhamasisha kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja kwani vikundi hivi husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi sasa tutumie fursa hiyo kwa kushirikisha vikundi vya jogging vilivyopo kwenye kata, mitaa au vijiji,” amesisitiza Majaliwa

Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zote nchi kuhakikisha zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi yaliyopo kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi waweze kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi na wanafunzi kukimbia mchaka mchaka kabla ya kuingia darasani ili kujiimarisha kiafya.

Amesisitiza kuwa taarifa za shirika la maendeleo Duniani (UNDP) za mwaka 2013 zinaonesha bado magonjwa hayo yasiyoambukiza yanaathiri nyanja nyingine za maisha kwani inakadiriwa katika kipindi cha miaka 20 kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya zitafikia Dola za Marekani trilioni 47.

Awali Waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto.Ummy Mwalimu amesema magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha magonjwa ambayo hayawezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Ameyataja magonjwa hayo kuwa ni pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho, kinywa, masikio, pua na koo na kwamba yamekuwa yakiongezeka duniani kote na kuathiri kimaisha.

Waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwa mwaka 2016 hadi wagonjwa milioni 4.2 mwaka 2018 sawa na ongezeko la asilimia 24.

MOI yafanikisha upasuaji mtoto mwenye kifafa
Wizara yataka ushirikiano kupandisha hadhi ya chai