Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa katika hospitali ya Ruangwa na kusema kuwa gari moja litabaki katika Hospitali hiyo ya Wilaya na lingine litapelekwa katika kituo cha afya cha Mandawa.

Majaliwa amekabidhi magari hayo mapema hii ikiwa ni siku ya tatu tangu aanze ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, ambapo amesema kuwa huo ni mkakati na muendelezo wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwasogezea na kuboresha huduma kwa wananchi wake.

Aidha, amesema kuwa magari hayo ni ya kisasa na yatarahisisha usafiri kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharula katika hospitali kubwa kitu ambacho kitawaondolea wananchi kero mbalimbali zikiwemo huduma za afya.

“Rais wetu Dkt. Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero hivyo mkakati huu ni wa nchi nzima, ndio maana sisi tunafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunaondoa kero kwa wananchi wetu,”amesema Majaliwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya amesema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri kwa wagonjwa wa dharula.

Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Regan Rajuu amesema hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo umeongezeka kutoka asilimia 80 Desemba, 2016 na kufikia asilimia 90 Juni 2017.

 

Kisela yaikimbiza wasikudanganye na Eneka ya Diamond
Ng'ombe 165 wasafirishwa kwa ndege kwenda Qatar