Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  amekagua ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic katika kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga, Pwani.

Majaliwa amesema Serikali itahakikisha viwanda vinajengwa kwa wingi nchini kwani ndiyo msingi imara wa ukuaji wa uchumi na muarobaini wa tatizo la ajira hususan kwa vijana.

“Mbali na kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini, viwanda hivi ndivyo vitakavyotufanya tununue bidhaa kwa bei nafuu tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa vitu vingi vinaagizwa kutoka nje ya nchi,” – Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa kiwanda hicho cha kutengeneza vigae.

Katika ukaguzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. Frank Yang alisema jumla ya ajira 4,500 zinatarajiwa kutolewa kiwandani hapo mara ujenzi utakapokamilika.

Akifafanua kuhusu ajira hizo Bw. Yang alisema ajira 1,500 zitakuwa rasmi na zisizo rasmi zitakuwa 3,000 huku wakazi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho wanatarajiwa kupewa kipaumbele.

Mkurugenzi huyo alisema ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu dola milioni 100 na utafanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

“Ujenzi wa kiwanda hiki utainua ukuaji wa uchumi nchini Tanzania kwani utakapokamilika Serikali itakusanya sh. bilioni 30 kwa mwaka ikiwa ni mapato ya kodi,” alisema.

 

Sasa Ni Rasmi: Wales Yaipiku England Viwango Vya Soka Duniani
Zlatan Ibrahimovic Kuachwa Safari Ya China