Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa amechukizwa na biashara za magendo zinazoendelea katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, hivyo amewataka viongozi wa wilaya hiyo wajipime wenyewe.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Kagera katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani humo kilichofanyika mjini Bukoba.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera, Adam Ntogha kumsimamisha kazi Afisa wa Forodha katika mpaka wa Mulongo. Peter Mtei kwa tuhuma za kujihusisha na biashara za magendo.

“Biashara za magendo zinafanyika bila ya wao kuchukua hatua, mnatia aibu yaani hakuna kazi inayofanyika. Viongozi wa wilaya ya Kyerwa mjipime wenyewe, mialo mingi katika wilaya yenu inatumika kwa biashara ya magendo na butura,”amesema Majaliwa

Aidha, ameongeza kuwa katika mwalo wa Mulongo uliopo kwenye eneo ambalo Tanzania inapakana na nchi za Uganda na Rwanda, biashara za magendo na butura zinafanyika na hakuna kiongozi yeyote anayechukua hatua.

Hata hivyo, katika hatua nyingine, Majaliwa amemtaka Meneja wa TRA asiwahamishe watumishi wabovu kutoka kituo kimoja cha forodha na kuwapeleka kingine kwa kuwa huko wanakowapeleka wanakwenda kuendeleza biashara za magendo na kuikosesha Serikali mapato.

 

Video: Tundu Lissu atoboa majanga ya Mbowe, Jinamizi la MV Nyerere latanda
Kimbunga Michael kuikumba Marekani