Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ardhi  uliodumu kwa miaka 17 kati ya vijiji viwili vya Ortukai na Esilalei na Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) baada ya kukabidhi hati ya  shamba la Manyara Ranch  kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya.

Majaliwa ametoa hati hiyo jana Desemba 4, 2016 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Mto wa Mbu kwenye viwanja vya Barafu baada ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji  hivyo vilivyopo kwenye  Kata ya Elesilalei Wilayani Monduli Mkoani Arusha.

Majaliwa amechukua uamuzi huo kufuatia kilio cha muda mrefu cha wananchi hao kudai kuwa Rais wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliagiza shamba hilo ligaiwe kwa wananchi hao lakini jambo hilo halikufanyika na badala yake watu wachache walijimilikisha shamba hilo kinyemela chini ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.

Amesema Serikali imeamua kurudisha umiliki wa shamba hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili baada ya Baraza la Madiwani na Uongoziwa Wilaya hiyo ya Monduli kuridhia kwa pamoja umiliki huo kurudi kwa wananchi kama ilivyoamriwa hapo awali.

“Shamba hili lenye ukubwa wa ekari 44,930 sasa si mali tena ya Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) iliyokuwa inafadhiliwa na Shirika la African Wildlife Foundation (AWF) sasa ni mali ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya Monduli ndio itapanga matumizi bora ya ardhi ya shamba hili mliloteseka nalo kwa muda mrefu ,” alisema.

Pamoja na hayo, majaliwa amesema Serikali inaendelea kufuatilia maeneo yote yaliyochukuliwa na watu bila ya kuyaendeleza na kuwapa wananchi. “Ni kwa nini watu wenye fedha wanachukua mashamba mkubwa bila ya kuyaendeleza huku wananchi wakiteseka kwa kukosa maeneo ya kilimo na ufugaji,” alisema.

Kabla ya kuhutubia mkutano huo wa hadhara Majaliwa alitembelea shule ya msingi ya Laiboni iliyoanzishwa  na mzee maarufu wa kimila wilaya huko Laigwanani Meshuko Ole Mapii ambayo inawanafunzi 102 wakiwemo wajukuu na watoto wa mzee  ambapo alitangaza umiliki wa shamba hilo kurudi kwa wananchi.

 

Makampuni matano ya Manji yang'olewa quality plaza
Mpango: Epukeni rushwa na ufisadi