Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mara kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi Mtendani wa Mamlaka ya Maji Musoma (MUWASA) Mhandisi Gantala Said kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji Bunda.

Mbali na Mkurugenzi huyo pia ameiagiza TAKUKURU kumhoji Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Nyakirang’anyi, Mahuza Mumay ambaye ndiye mkandarasi anayejenga mradi huo unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye eneo la Nyabehu hadi Bunda mjini.

Amefikia uamuzi huo baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kueleza sababu zilizosababisha mradi wa maji Bunda kutokamilika pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi.

Aidha, Majaliwa amesema kuwa kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo  inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.

Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ameagiza kufungwa kwa ofisi za MUWASA na kuwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoruhusiwa kuingia ofisini hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

 

Mailu ataka ripoti hospitali inayodhalilisha wanawake kingono
ZANU-PF yawafukuza wabunge 11