Jumamosi, 10 Septemba, 2016 katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kagera, Mwanza na Mara limetokea tetemeko lililosababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa jana ameongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba mjini, Kagera kuaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko hilo la ardhi lililotokea.

Waziri Mkuu alimuwakilisha Rais, John Magufuli ambapo amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.

“Poleni sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu  Serikali ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” – Majaliwa

Majaliwa amesema Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo na hayafai kutumika.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi kulala uwanjani.

Pia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetakiwa kuangalia kama kuna tetemeko linguine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu amesema kwa sasa wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba zao zimeanguka. Pia mkoa unaendelea kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Kabla ya hayo, Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako majeruhi 170 wamelazwa na kutoa pole na kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hoispitali kubwa Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.

  • —>> Tetemeko dogo la ardhi limetokea tena jana majira ya saa nne usiku katika mkoa wa Kagera na kuzusha hofu kwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba ambao iliwalazimu wengine kulala nje kuhofia uhai wao.

Habari kutoka mkoani Kagera zinasema kuwa tetemeko hilo halikuwa kubwa kama lililotokea siku ya Jumamosi ambalo lilisababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa.

Tetemeko hilo la awali pia lilisababisha kubomoka kwa nyumba 840 huku nyingine 1,264 zikiachwa na nyufa na mabweni ya shule ya sekondari Nyakato yakiharibika kabisa kulikopelekea wanafunzi kukosa mahali pa kulala.

Awali akiongea mara baada ya kutembelea waathirika wa tetemeko hilo Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wakazi ambao nyumba zao zimeharibiwa kutorejea kwenye nyumba hizo kwa kuwa bado haijajulikana kama tetemeko hilo litajirudia au la

Wabunge wa Ukawa wasusia Mechi na viongozi wa dini kumkwepa Makonda, Dk Tulia
Nahreel afichua siri ya 'Roma' kutoka Kimuziki, alichangia bila kumjua