Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. milioni 190 kutoka kwa balozi wa Pakistan nchini. Amir Khan, Kaimu Balozi wa China Mhe. Gou Haodong na Taasisi ya Aga Khan kwa ajili ya kusaidiia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.
Waziri Mkuu amekabidhiwa michango hiyo leo Septemba 30, 2016 kwenye Hotel ya Hyatt Regency jijini Dar Es Salaam ambapo amewashukuru kwa michango hiyo na alitumia fursa hiyo kuwaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao kwa kuipeleka ofisini kwake au kutuma kupitia akaunti ya maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz
Majaliwa amesema watu walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kupokea michango ya maafa hayo ambazo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Balozi wa Pakistan, Amir alisema wanaamini mchango huo wa sh. milioni 80 walioutoa utasaidia kuwapunguzia uchungu wananchi wa Kagera kutokana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi.
Mbapo Kaimu Balozi wa China, Haodong amemweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na tayari walishawapeleka madaktari na wataalamu wengine mkoani Kagera na leo walikuwa wanakamilisha ahadi yao ya kutoa mchango wa sh. milioni 60.
Aidha, Muwakilishi Mkazi wa Taasisi za Aga Khan nchini, Amin Kurji alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 50.