Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa mabati 100 yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni mbili kutoka kwa Mbunge wa Viti maalum mkoa  wa Lindi, Hamida Abdallah.

Majaliwa amepokea msaada huo leo Oktoba 19, 2016 katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara  yake hospitalini hapo, ikiwa msaada huo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mbunge wa Viti maalum, Hamida mwezi Aprili mwaka huu wakati Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Hospitali hiyo.

Mbunge Hamida wakati akikabidhi msaada huo amesema Waziri Mkuualipofanya ziara ya mwezi wanne hospitalini hapa nilikuahidi kukupa mabati  100 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanawake. Nilitoa ahadi hii baada ya kuona jitihada kubwa unazozifanya katika kuimarisha hospitali hii,” amesema.

Akipokea msaada huo Waziri Mkuu amemshukuru Mhe. Hamida kwa kutekeleza ahadi yake na kumuomba aendelee kuisaidia hospitali hiyo pindi anapopata nafasi.” Nashukuru sana kwa msaada wako tunajua kutoa ni moyo na si utajiri,”.

Waziri Mkuu amesema mkakati wake kwa sasa ni kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kuwawezesha wananchi kupata matibabu karibu na makazi yao.

“Nataka sekta ya afya inapata mafanikio makubwa. Nitashirikiana na wananchi  kuhakikisha kunakuwa na zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya kwenye kata zote,” – Majaliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue amemshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kuboresha huduma hospitalini hapo.

Amesema hivi karibuni walipokea sh. milioni 100 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi kwa ajili ya ukarabati wa wodi mbili ambazo tayari ukarabati huo umekamilika na zitaanza kutumika kuanzia Novemba 15 mwaka huu.

TFF Yaitahadharisha Toto Africans
Ikulu yakanusha taarifa ya kutenguliwa kwa uteuzi wa RC Gambo