Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameendelea kupokea michango kutoka kwa wadau mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Kagera ambapo leo amepokea fedha taslimu sh. milioni 25.62 pamoja na nguo zenye thamani ya sh. milioni mbili.

Majaliwa amepokea michango hiyo leo Oktoba 14, 2016 kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sh. milioni 20, Mtandao wa Wasanii Tanzania sh. 620,000 na nguo mifuko miwili, Chama cha Makatibu Mahsusi (TAPSEA) sh. milioni tano.

Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amewashukuru wote wanaotoa michango na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

“Nawashukuru kwa kuamua kutumia siku ya leo ya kukumbuku ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwachangia wenzetu waliopatwa na maafa,” amesema.

Wengine waliomkabidhi michango Waziri Mkuu ni Umoja wa Wafanyabiashara Ndogondogo soko la Kariakoo ambao wametoa marobota mawili ya nguo (suruali, kanzu na nguo za akinamama na moja la wanasesere kwa ajili ya watoto waliopatwa na maafa vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni mbili.

 

Manispaa ya Ilala Wamuenzi Baba wa Taifa kwa Kufanya Usafi
Mwalimu atekwa na kutishiwa aache ufuatiliaji