Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka washiriki wa kozi fupi ya viongozi, kutambua, kufuata na kusimamia falsafa ya Serikali iliyojielekeza katika kuwahudumia watanzania.

Majaliwa ameyasema hayo, hiyo leo Agosti 2, 2022 wakati akifungua kozi fupi ya 13 ya viongozi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Dar Es Salaam, ya kuwaongezea uelewa na ufanisi katika eneo zima la ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa.

Amesema, Serikali inatarajia kuona mabadiliko ya kimtazamo, ushauri na maamuzi watakayoyafanya yanapaswa kuakisi walichokipata kupitia kozi hiyo mara baada ya viongozi hao kurudi kwenye maeneo yao ya utendaji.

“Serikali inatarajia kwamba washiriki wote, watatumia kikamilifu fursa hiyo adhimu kushiriki kwa umakini na uhodari wa hali ya juu ili kuongeza uelewa wao wa masuala mtambuka hususan ya kiulinzi, kiusalama na kistratejia,” amesema Wazir Mkuu.

Amesema, “Sisi viongozi wenu tunatarajia kuona kuwa mtakapohitimu mafunzo haya mtakuwa mmebadilika kimtazamo na hilo halinabudi kujidhihirisha kwa Wizara na Taasisi mnazotoka kuzungumza lugha moja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi yetu.”

Aidha ameongeza kuwa, “Kwa kufanya hivyo, mtasaidia sana kusukuma maendeleo ya nchi yetu kwa haraka hasa katika kipindi hiki ambapo Serikali inalenga kukuza uchumi wa viwanda. Sambamba na hilo, tunapaswa kutambua kwamba changamoto za sasa ni mtambuka na si rahisi kutatuliwa na Wizara au Taasisi moja moja.”

Awali, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema chuo hicho tangu kianzishwe Septemba 2012 kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kutoa kozi ndefu 10 pamoja na kozi fupi 12.

Amesema “Mafanikio mengine yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na kujitangaza na kukubalika kimataifa ambapo viongozi kutoka mataifa 16 wamehudhuria kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo.”

Kwa upande wake, Kansela wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Balozi Dkt. Marten Lumbanga amesema mafunzo hayo yanayotolewa kwa viongozi yataleta matokeo chanya kwa washiriki na kulifanya Taifa lisonge mbele na salama kwani wataongezewa ueleewa na umakini katika usimamizi madhubuti wa sera kwa usalama wa nchi.

Kozi hiyo imehudhuriwa na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Waandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi za Kimkakati za Serikali.

Shaban Kaoneka amtangazia vita Dullah Mbabe
Waziri Aweso atoa bei elekezi ya maji